Kamati inayochunguza mauaji ya Shakahola yaomba muda zaidi

Marion Bosire
1 Min Read

Kamati maalumu ya bunge la Seneti iliyobuniwa kuchunguza mauaji ya Shakahola inaomba muda zaidi ili iweze kukamilisha kazi yake.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Seneta wa kaunti ya Tana River Danson Mungatana anasema bado wanakusanya ushahidi na maoni ya wakenya kwa hivyo wakenya wawe na subira.

Mungatana alikuwa akizungumza katika eneo bunge la Garsen, wakati wa hafla ya kuzindua Biblia iliyotafsiriwa kwa lugha ya Pokomo.

Kamati hiyo maalumu ya wanachama 11, ilibuniwa ili kubaini namna mhubiri Paul Mackenzie alihadaa wafuasi wake wengi kufunga kula na kunywa na kisha kufariki na kuzikwa katika msitu wa Shakahola.

Mackenzie alikamatwa Aprili 15, 2023 na amesalia korokoroni tangu wakati huo pamoja na wenzake 28.

Awali kamati hiyo iliongezewa siku 30 zaidi baada ya miili zaidi kufukuliwa na ilifaa kuwasilisha ripoti kamili bungeni Septemba 15, 2023.

Miili zaidi ya 400 imefukuliwa kutoka msitu wa Shakahola na uchunguzi wa nyingi za maiti ulibaini kwamba wahasiriwa walifariki kutokana na njaa.

Share This Article