Mabalozi tisa wanaowakilisha nchi mbalimbali za kigeni wamesitisha kimya chao na kulalamikia visa vinavyoongezeka vya watu kutekwa nyara kiholela na kupotea humu nchini.
Hii ni licha ya mahakama awali kutoa uamuzi unaotaja visa kama hivyo kuwa kinyume cha sheria.
“Tunaelezea wasiwasi wetu juu ya ripoti zinazoendelea za watu kukamatwa kiholela na kutoweka wasijulikane waliko licha ya kuwepo kwa maamuzi ya Mahakama Kuu. Tunafahamu ahada ya Rais William Ruto kuwa visa kama hivyo havitatokea tena chini ya utawala wake na kwamba watu wote wanaohusika watawajibishwa,” walisema mabalozi hao kwenye taarifa leo Alhamisi.
“Uchunguzi wa haraka na wa wazi utaiwezesha Kenya kudhihirisha kwa ulimwengu kujitolea kwake kulinda haki wakati ikichukua kiti chake kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.”
Mabalozi wa nchi za Uingereza, Denmark, Ufini, Ujerumani, Ireland, Uholanzi, Norway, Uswidi na Uswizi wametia saini taarifa hiyo.
Marekani ni miongoni mwa ambazo hazikutia saini.
Taarifa hiyo inakuja wakati kumekuwa na idadi inayoongezeka ya visa vya kamatakamata nchini, wa hivi karibuni zaidi akiwa mwanaharakati Boniface Mwangi ambaye aliachiliwa hivi majuzi.
Kwa upande mwingine, Mwanablogu Maverick Aoko hajulikani aliko baada ya kutoweka kwa njia ya kutatanisha.
Upinzani ukiongozwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka umeisuta serikali kutokana na kuongezeka kwa visa hivyo.