Kiongozi wa chama cha Wiper ambaye pia ni mmoja wa viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Kalonzo Musyoka amesema kwamba atawania Urais mwaka 2027 baada ya kuchukua uongozi wa muungano huo.
Kalonzo alikuwa akizungumza huko Mombasa kwenye tamasha ya jamii ya Akamba iliyohudhuriwa na viongozi kadhaa wa upinzani ambapo alisema yuko tayari kupambana na Rais William Ruto kwenye uchaguzi ujao.
Alimlaumu Rais kwa kutumia urafiki wake na Raila Odinga kuendeleza ushawishi wake kisiasa katika eneo la Nyanza.
Kulingana naye, wafuasi wa muungano wa Azimio wamemchagua kuwania Urais kwenye uchaguzi ujao, matamshi yaliyoungwa mkono na kiongozi wa chama cha Jubilee Jeremiah Kioni.
Kioni alifafanua kwamba Kalonzo ataongoza oparesheni kwa jina “Okoa Kenya” na ni wakati kila mmoja amtambue kama kiongozi rasmi wa upinzani.
Kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa naye aliongeza kusema kwamba iwapo wanachama wa ODM wana kiongozi mwingine wamlete akisisitiza kwamba Kalonzo amesimama na Raila mara tatu.
Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Sharrif Nassir ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama cha ODM alisisitiza kwamba chama hicho bado kiko kwenye muungano wa upinzani Azimio.