Kalonzo ataka watu waliotekwa waliosalia kuachiliwa huru

Wengi wamekuwa wakilalamikia visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara nchini. Mamlaka zinasema visa hivyo vinafanyiwa uchunguzi kwa sasa.

Martin Mwanje
1 Min Read
Kalonzo Musyoka - Kinara wa chama cha Wiper

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ametoa wito wa kuachiliwa kwa watu waliosalia waliotekwa nyara. 

Anautuhumu utawala wa sasa kwa utekaji huo.

Akiwahutubia wanahabari leo Jumatano, Kalonzo ameitaka serikali ya Kenya Kwanza kufanya kila iwezalo kukomesha visa vya utekaji nyara nchini na wakati huohuo kuheshimu utawala wa sheria.

Matamshi yake yanakuja huku Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja akiwa ameagizwa kufika mahakamani Januari 27 mwaka huu kuhusiana na visa vya utekaji nyara.

Agizo la kumtaka Kanja kufika mahakamani lilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye.

Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi pia amejitosa kwenye mdahalo huo akilalamikia kuongezeka kwa visa vya utekaji nyara nchini.

Ametaja kutekwa kwa mwanawe mwaka jana kuwa kisa kilichomfadhaisha mno.

Muturi alifika katika ofisi za Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI jana Jumanne na kuandikisha taarifa kuhusiana na kisa hicho.

Inspekta Mkuu wa Polisi amekanusha vikali kuhusika kwa maafisa wake katika utekaji huo.

Watano kati ya vijana sita waliokuwa wametekwa nyara wamepatikana hadi kufikia sasa.

Kule Mlolongo, kaunti ya Machakos, kunazo familia za wanaume wanne walioripotiwa kutekwa nyara ambazo pia zinapasa sauti.

Zimetoa wito kwa mamlaka husika kuingilia kati na kuhakikisha wanao wanaachiliwa huru.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *