Mwanamuziki Jose Chameleone anaomboleza kifo cha kakake mkubwa kwa jina Humphrey Mayanja. Chameleone alichapisha picha ya Humphrey kwenye akaunti yake ya Instagram na kuweka ishara za kuonyesha kwamba analia.
Alichapisha pia video inayomwonyesha marehemu Humphrey akicheza gitaa na kuandika maneno, “Lala Salama Humphrey Mayanja”.
Humphrey ndiye mkubwa katika familia ya wanamuziki hao Chameleone, Pallaso, Weasel na marehemu AK47 ambaye aliaga dunia mwaka 2015.
Anaripotiwa kupoteza maisha kutokana na maradhi ya saratani ambayo yaligunduliwa nchini Marekani Julai mwaka jana, wakati huo yeye na Jose walikuwa wanaugua huko huko Marekani.
Baba ya wawili hao Gerald Mayanja alihojiwa wakati huo ambapo alifichua kwamba Humphrey aliyekuwa analalamikia maumivu makali ya tumbo aligunduliwa kuwa na saratani ya utumbo ambayo ilikuwa imekolea.
Mzee huyo anaelezea kwamba waliamua kama familia kumrejesha nyumbani Uganda ambapo amekuwa akipokea matibabu hadi kifo chake.