Kabogo apendekeza matumizi ya sheria kukabiliana na changamoto ibuka za teknolojia

Alisema hayo mbele ya kamati ya bunge ya usaili, inayotathmini ufaafu wake wa kuhudumu kama waziri.

Marion Bosire
2 Min Read

William Kabogo ambaye aliteuliwa na Rais William Ruto kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali amependekeza matumizi ya sheria zilizopo na nyingine zitakazobuniwa, kukabiliana na changamoto ibuka za kiteknolojia.

Alikuwa akijibu swali la Naibu Spika wa Bunge la Taifa Gladys Shollei ambaye pia ni Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Usaili aliyetaka kujua hatua ambazo atachukua kama Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali, kusimamia usambazaji wa habari za uwongo na maudhui mabaya mitandaoni.

Hatua ya kwanza kulingana naye ni kutumia sheria zilizopo za kudhibiti matumizi ya tarakilishi nchini, kubuni sheria iwapo zitahitajika na kuwasiliana na wanaoeneza habari na maudhui mabaya.

Alitoa mfano wa iwapo mtu atachapisha picha yake akiwa kwenye jeneza, atawasiliana naye kufahamu angehisi vipi iwapo yeye mwenyewe angefanyiwa hivyo.

Kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah alitaka kufahamu hatua atakayochukua Kabogo kukabiliana na hatua ya kampuni kubwa za nchi kama Marekani zinazonyanyasa wakenya kwa kuwapa kazi mitandaoni na kuwapila hela kidogo kama dola mbili kwa saa.

Kabogo alisema anatumai kuwasilisha bungeni mswada ambao utaweka kiwango cha malipo yanayotarajiwa kwa kazi za mitandaoni ikiwemo kazi ya kuunda maudhui.

Gavana huyo wa zamani wa kaunti ya Kiambu aliahidi pia kuandaa mchakato wa kufuatilia mawasiliano ya simu za rununu ili kuhakikisha kwamba kila mteja anapata huduma bora sambambana pesa anazolipa.

hatua hiyo itahakikisha pia, serikali imefahamu muda wa maongezi ya simu unaouzwa na kampuni hizo ili kuweza kufahamu kiwango kamili cha ushuru ambao zinafaa kulipa.

Kuhusu wadhifa wa kiongozi wa chama cha Tujibebe, Kabogo alisema kwamba alijiuzulu siku moja baada ya kuteuliwa na Rais Ruto kuwa Waziri na kwamba ana stakabadhi za kuthibitisha.

Leo Jumanne, kamati ya bunge kuhusu uteuzi inawasaili watu watatu walioteuliwa na Rais Ruto  kuwa mawaziri.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *