KAA yawataka wasafiri kuwasili mapema JKIA

Martin Mwanje
2 Min Read

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini, KAA umewataka wasafiri kuhakikisha wanawasili mapema katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA ili wasichelewe kuabiri ndege na kuelekea waendako. 

Hii kwa sababu ya ukaguzi na taratibu zilizoimarishwa zaidi katika uwanja huo kufuatia tishio la vijana wa Gen Z la kufika uwanjani hapo na kutatiza shughuli za usafiri.

“Kutokana na ukaguzi wa usalama na taratibu zilizoimarishwa JKIA, abiria wanashauriwa kuwasili katika uwanja huo mapema ili kuepukana na uwezakano wa kukosa kupata ndege zao,” ilisema ilani ya KAA kwa umma.

“Tafadhali wasiliana na shirika lako la ndege kwa taarifa za hivi punde zaidi. Safiri salama.”

KAA ilitoa wito huo wakati ambapo Kaimu Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja amewataka waandamanaji kuhakikisha wanaepuka kwenda katika maeneo yasiyoruhusiwa.

“Kwa kuzingatia maandamano yaliyopangwa kufanywa Julai 23, 2024, ni muhimu kuukumbusha umma mipaka ya kisheria inayosimamia maeneo yanayolindwa,” alisema Kanja katika taarifa.

“Sheria ya maeneo yanayolindwa kifungu cha 204 cha sheria za Kenya inazuia watu wasioruhusiwa kuingia maeneo ambayo yametangazwa kuwa yanayolindwa.”

Ametaja maeneo hayo kuwa yanayojumuisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA.

Usalama umeimarishwa maradufu katika maeneo yanayolindwa ikiwa ni pamoja na majengo ya bunge na Ikulu ya Nairobi wakati vijana wa Gen Z wakipanga kuandamana leo Jumanne.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *