Waziri Mkuu Justin Trudeau ameomba msamaha kwa niaba ya Canada baada ya mwanaume mmoja wa Ukraine aliyepigana katika kitengo cha Nazi kupigiwa makofi kimakosa bungeni.
“Hili ni kosa ambalo liliaibisha sana bunge na Canada,” Bw Trudeau alisema Jumatano.
Spika Anthony Rota, ambaye alichukua jukumu la kumwalika Yaroslav Hunka, mwenye umri wa miaka 98, alijiuzulu Jumanne.
Tukio hilo limelaaniwa kimataifa.
Bw Trudeau pia aliomba msamaha moja kwa moja kwa kiongozi wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye alikuwa akiizuru Canada na kuhudhuria bungeni, akisema: “Canada inasikitika sana.”
Kiongozi huyo wa Ukraine alikuwa miongoni mwa wale waliopigwa picha wakimshangilia Bw Hunka, picha ambayo imekuwa ikitumiwa katika propaganda za Urusi.