Justin Muturi afutwa kazi kama Waziri wa Utumishi wa Umma

Martin Mwanje
1 Min Read
Justin Muturi - Waziri wa Utumishi wa Umma anayeondoka

Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi amefutwa kazi.

Muturi ametemwa na Rais Ruto katika mabadiliko ya hivi punde yaliyofanywa katika Baraza la Mawaziri.

Kwenye mabadiliko hayo, ni Geoffrey Kiringa Ruku atakayejaza pengo lililoachwa na Muturi baada ya kuteuliwa kuwa Waziri mpya wa Utumishi wa Umma.

Muturi, ambaye alihudumu kama Mwanasheria Mkuu kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Utumishi wa Umma, amekuwa katika mstari wa mbele kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza kutokana na visa vya utekaji nyara nchini.

Isitoshe, alitoa wito wa kubuniwa kwa tume ya uchunguzi ili kutegua kitendawili cha ni nani wanaotekeleza visa hivyo na kutaka wahusika kuwajibishwa.

Muturi alikuwa mwathiriwa baada ya mwanawe kutekwa nyara na watu wasiojulikana kabla ya kuachiliwa huru mwaka jana.

Ni hali iliyomfanya kulalamikia kuongezeka kwa visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela aliyosema ni jambo linalozitia hofu familia nyingi na kumtaka Rais William Ruto kuingilia kati na kukomesha jinamizi hilo.

Msimamo wa Muturi uliwafanya wachanganuzi wa mambo kukisia kuwa haitachukua muda mrefu kabla ya Waziri huyo kupigwa kalamu.

Macho sasa yanaangazia mustakabali wa Muturi ambaye kuna makisio kuwa huenda akagombea ugavana katika kaunti ya Embu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Website |  + posts
Share This Article