JSC yasitisha kuajiriwa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufaa

Martin Mwanje
2 Min Read

Tume ya Huduma za Mahakama, JSC imesitisha kuajiriwa kwa Majaji 11 wa Mahakama ya Rufaa kutokana na changamoto za kifedha. 

Mchakato wa kuwaajiri Majaji hao ulipangwa kuanza leo Jumatano.

Aidha, JSC imesitisha kuajiriwa kwa maafisa wengine wote wa Idara ya Mahakama.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatano, Jaji Mkuu amesema hatua hiyo imetokana na kupunguzwa kwa fedha ilizotengewa idara hiyo.

“Tume ya Huduma za Mahakama, JSC imepokea taarifa kutoka kwa Wizara ya Fedha Namba 6/2024 iliyoandikwa tarehe 28 mwezi Juni, 2024 ikielezea kuwekewa ukomo wa matumizi hadi asilimia 15 ya bajeti. Taarifa hiyo inaruhusu tu matumizi kwa huduma muhimu,” alisema Jaji Koome ambaye pia ni mwenyekiti wa JSC.

“Kwa misingi hii, tumelazimika kufanyia mabadiliko makubwa mipango na shughuli zilizoratibiwa. Kwa masikitiko, hii imeilazimisha JSC kuchukua uamuzi wa kusitisha kuajiriwa kwa maafisa wote wa idara ya mahakama wakiwemo Majaji 11 wa Mahakama ya Rufaa kulikoratibiwa kuanza leo.”

Kwa sasa, Mahakama ya Rufaa ina jumla ya Majaji 29 wanaohudumu katika vituo sita kote nchini.

Wakati akitangaza kuwa hatatia saini Mswada wa Fedha 2024, Rais William Ruto alisema nakisi ya fedha itakayotokana na kukataliwa kwa mswada huo itagharimiwa na serikali kuu, idara ya mahakama na bunge.

Mgao wa fedha kwa serikali za kaunti pia unatarajiwa kupunguzwa.

Makali ya kukataliwa kwa mswada huo sasa yakianza kudhihirika kutokana na hatua ya Idara ya Mahakama kusitisha kuajiriwa kwa maafisa wote wa idara hiyo.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *