Tume ya Huduma za Mahakama, JSC imewahakikishia Wakenya kwamba imeshughulikia madai yote ya ufisadi na utovu wa nidhamu yaliyowasilishwa kwake.
Hakikisho hilo linakuja wakati madai ya kukithiri kwa ufisadi miongoni mwa majaji yamewaka moto.
Akiwahutubia wanahabari leo Jumatatu, mwenyekiti wa tume hiyo ambaye pia ni Jaji Mkuu Martha Koome amesema JSC uhakikisha majaji na maafisa wa idara ya mahakama wanafahamu vigezo vinavyoongoza utendakazi wao wakati wa kuajiriwa kwao, ikiwa ni pamoja na kudumisha kanuni za haki na maadili ya idara ya mahakama.
“Ni msimamo thabiti wa JSC kwamba ufisadi au utovu wa nidhamu katika idara ya mahakama vinaangaziwa kwa kupewa kipaumbele. Tunashikilia msimamo kuwa udumishaji wa maadili katika utendakazi wa majukumu ya mahakama ni suala lisiloweza kujadiliwa na isitoshe ni msingi wa kupata haki,” alisema Jaji Koome.
“Ni hakikisho kwamba JSC imeendelea kushughulikia kwa njia thabiti madai yote ya ufisadi na utovu wa niadhamu yaliyowasilishwa kwake.”
Na ili kudhirisha utendakazi wake,tume ya JSC inasema mwaka wa 2023, ilipokea jumla ya malalamishi 72 dhidi ya majaji.
Malalamishi 13 yalipuuziliwa mbali kwani yalikuwa nje ya himaya yake. Majaji 6 walitakiwa kujibu malalamishi dhidi yao ilhali malalamishi 49 yanaendelea kufanyiwa tathmini ya awali na tume hiyo.
JSC ikiongeza kuwa majaji 3 waliondoka katika idara ya mahakama mwaka jana, mmoja akiamua kustaafu mapema na wawili wakiondolewa kufuatia mapendekezo ya jopo maalum.
Jaji Koome alilalamikia matishio ya uongozi wa serikali kuu na bunge kutoheshimu maagizo ya mahakama akitayataja kuwa hatari zaidi na shambulio kwa katiba.
Tume hiyo ikionya kuwa hatua kama hiyo inaweza ikasababisha mizozo ya kiraia.