Mwanamuziki wa Uganda Joan Namugerwa maarufu kama Jowy Landa, amemwomba Jenerali Salim Saleh msaada wa kifedha kugharamia matibabu ya kakake ambaye amelazwa hospitalini.
Akisimulia kuhusu kuugua kwa kakake, Jowy alifichua kwamba kakake amelazwa kwa muda wa miezi mitano sasa na hawezi kutumia sehemu za mwili wake inavyostahili.
Kulingana naye, kakake alipigwa kwenye vurugu na marafiki hadi akazimia.
Jowy anasema amekuwa akitumia shilingi milioni moja za Uganda kwa siku kugharamia matibabu katika chumba cha wagonjwa mahututi yaani ICU.
Ada hiyo imemzidi ikitizamiwa kwamba yeye ndiye anategemewa nyumbani kwake.
Sasa anaomba Jenerali Salim Saleh amsaidie kugharamia matibabu ya kakake ili apone arejelee maisha yake ya kawaida.
Msajiliwa huyo wa “Team No Sleep” amesema ametumia akiba yake yote kwa matibabu ya kakake huku mabadiliko yake yakiwa ya pole pole mno, kwani sasa kitu ambacho anaweza kufanya ni kufungua macho tu.
Salim Saleh ni mwanajeshi mstaafu wa Uganda kakake Rais Yoweri Museveni na sasa anahudumu kama mshauri wa Rais katika masuala ya wanajeshi.
Yeye huwa na ukaribu na wasanii wa Uganda na huwa anawasaidia mara kwa mara.