Jopo la majaji labuniwa kusikiliza kesi ya kupinga kuvunjwa kwa bunge

Marion Bosire
1 Min Read

Kitengo cha mawasiliano cha idara ya mahakama kimetangaza kubuniwa kwa jopo la majaji watano ambalo litasikiliza kesi zilizojumuishwa za kupinga kuvunjwa kwa bunge.

Jopo hilo lililobuniwa Julai 31, 2024 linajumuisha majaji Jairus Ngaah ambaye ni mwenyekiti, Lawrence Mugambi, Patricia Nyaundi, Moses Otieno na Tabitha Ouya Wanyama.

Kesi hizo ziliwasilishwa mahakamani mwaka 2020 baada ya aliyekuwa jaji mkuu wakati huo David Maraga, kumshauri Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta kuvunja bunge.

Ushauri wa Maraga kwa Rais Uhuru ulitokana na maombi sita ambayo alikuwa amepokea kutoka kwa wananchi ya ushauri kuhusu kuvunjwa kwa bunge kwa kukosa kuafiki mahitaji ya uwakilishi wa jinsia.

Sheria ya uwakilishi wa jinsia inaelekeza kwamba kusiwe na zaidi ya thuluthi mbili za watu wa jinsia moja katika taasisi mbali mbali za serikali likiwemo bunge.

Seeptemba 21, 2020 ndiyo siku Maraga alitoa ushauri wake kwa Rais Uhuru hatua iliyochochea kesi hizo ambazo zimejumuishwa na kuwa kesi moja.

Kesi hiyo itatajwa mbele ya jopo hilo la majaji watano mnamo Septemba 24, 2024.

Website |  + posts
Share This Article