Mwanamuziki wa Marekani Jennifer Lopez almaarufu JLO anaripotiwa kuondoka kwenye hafla ya uzinduzi wa filamu yake baada ya kuulizwa kuhusu P Diddy.
Lopez alikuwa amehudhuria hafla ya kuonyesha filamu iitwayo “Unstoppable” katika ukumbi wa maonyesho ya filamu ya TCL huko Los Angeles.
Hafla hiyo ilihusisha pia maswali kutoka kwa mashabiki na kuwatilia sahihi yake halisi alipoulizwa na mmoja atoe maoni kuhusu Diddy ambaye anazuiliwa na polisi kwa makosa yanayohusiana na ulanguzi wa binadamu ili kuwatumia kingono.
Video iliyosambazwa mitandaoni inamwonyesha JLO nje ya ukumbi wa TCL akiwa mwenye furaha huku akiwatilia sahihi mashabiki, alipofikia huyo mmoja aliyemuuziliza kuhusu Diddy, uso wake ulibadilika ghafla akakasirika na kuondoka pamoja na waliokuwa nao.
JLO na Diddy waliwahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa muda wa miaka miwili tangu mwaka 1999, baada ya kukutana kwenye uandaaji wa video ya wimbo wake “If You Had My Love”.
Uhusiano wao ulighubikwa na kashfa nyingi za ukosefu wa uaminifu na hata kuhusika kwenye kisa cha ufyatulianaji risasi katika eneo la burudani wakaishia kukamatwa na polisi.
Mashtaka dhidi yao hata hivyo yalitupiliwa mbali na walitengana mwaka 2001.
Hatua ya Lopez ya kukasirishwa na kutajwa kwa Diddy imewafanya wengi mitandaoni washangae iwapo anajua lolote kuhusu mashtaka dhidi ya Diddy ambaye amenyimwa dhamana.