Jimmy Nuru Angwenyi ameapishwa rasmi kama mwenyekiti wa baraza la kitaifa la mashujaa leo.
Hafla fupi ya kuapishwa kwake iliongozwa na jaji mkuu Martha Koome katika mahakama ya upeo hapa Nairobi.
Jaji mkuu alipongeza wawili hao kwa uteuzi wao akisema ana imani katika uwezo walionao wa kuimarisha kuafikiwa kwa malengo ya baraza la mashujaa.
Aliwasihi wakumbuke kwamba nyadhifa ambazo wameteuliwa kuhudumu ni zaidi ya jina na cheo. Ni ahadi kwa nchi hii kuendelea kuimarisha haki za mashujaa.
Awali Jimmy alihudumu kama mbunge wa eneo la Kitutu Chache kati ya mwaka 1997 na 2007, akaacha siasa kwa muda na aliporejea kwenye siasa mwaka 2013, eneo hilo likawa limegawanywa mara mbili.
Kitutu Chache Kaskazini na Kitutu Chache Kusini.
Alichaguliwa kama mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini mwaka huo wa 2013 hadi 2017.
Aliteuliwa na waziri Aisha Jumwa kwa wadhifa huu mpya ambapo atahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mwingine aliyeapishwa leo ni Rev David Lebarleyia ambaye atakuwa akihudumu kama mwanachama wa baraza hilo.
Baraza la kitaifa la mashujaa ni shirika la serikali ambalo liliasisiwa kupitia kwa sheria ya mashujaa wa Kenya nambari 5 ya mwaka 2014 kwa mujibu wa sheria ya mashirika ya kiserikali.
Linajukumiwa kuunda mwongozo wa kuchagua, kutambua na kutunuku mashujaa wa humu nchini kwa lengo la kuimarisha utaifa kupitia kutambua mchango wa mashujaa hao kwa nchi hii.