Jeshi la ulinzi la Jamuhuri ya Tanzania, leo Jumapili liliadhimisha miaka 60, tangu kubuniwa kwake Septemba 1, 1964.
Sherehe hiyo iliandaliwa katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salam, na kuhudhuria na maelfu ya wanajeshi, huku wakionyesha zana zao za kivita.
Katika hotuba yake kwa wanajeshi hao, Rais wa taifa hilo Samia Suluhu Hassan, aliwapongeza kwa kujitolea kwao mhanga kuilinda Tanzania, akiwaahidi kuwa atawaunga mkono kikamilifu kwa vyovyote vile.
“Katika siku ya leo tunayo kila sababu ya kujivunia kama Watanzania kwa kuendelea kuwa na Jeshi imara, la ulinzi, lenye weledi, utayari na nidhamu ya hali ya juu na linaloheshimika ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu,” alisema Rais Samia.
Kiongozi huyo wa Tanzania, aliwatambua watangulizi wa jeshi hilo wakiwemo marais wa zamani, akiwataja wazalendo wa kupigiwa mfano.
“Katika siku hii pia tunawakumbuka na kuwaenzi Marais na Maamiri Jeshi Wakuu waliopita, Wakuu wa Majeshi, Makamanda na Wapiganaji wote waliotangulia mbele za haki tunapoadhimisha miaka sitini ya chombo hiki walichokipenda na kukithamini sana,” aliongeza Rais huyo.
Aliwahimiza wanajeshi wa taifa hilo kuendelea kukumbatia nidhamu na kuilinda nchi yao kwa vyovyote vile.
“Ilindeni imani hiyo kwa nguvu kubwa, tena kwa nguvu kubwa sana. Endeleeni kufanya kazi zenu mkijua kwamba Amiri Jeshi Mkuu nipo nanyi kwa hali zote,” alisema Rais Samia.