Jean-Marc Kabund ahukumiwa miaka 7 kwa kumtukana Rais

Marion Bosire
2 Min Read
Jean-Marc Kabund

Jean-Marc Kabund ambaye ni mwaniaji urais nchini DR Congo alihukumiwa kifungo cha miaka 7 gerezani kwa makosa 12 yanayohusiana na kumtukana Rais wa nchi hiyo.

Alihukumiwa kifungo hicho kwa makosa kama kumtukana Rais, kudunisha idara za serikali na kueneza uvumi. Hukumu hiyo ya miaka 7 gerezani mawakili wake wanasema ni ya kiwango cha juu zaidi lakini inawiana na maombi ya upande wa mashtaka ambao ulitaka Kabund afungwe kwa zaidi ya miaka mitatu gerezani.

Kabund alikuwa kiongozi wa chama cha Union for Democracy and Social Progress – UDPS, ambacho ndicho chama cha Rais wa nchi hiyo Félix Tshisekedi.

Julai 2022, Kabund alitangaza kubuniwa kwa chama chake kiitwacho “Alliance for Change” na katika harakati hizo akakosoa chama tawala akisema kilikuwa kimekosa maono, viongozi wake hawakuwa na uwezo wa kuongoza nchi na kwamba kulikuwa na usimamizi mbaya katika idara mbali mbali za serikali.

Alikamatwa Agosti 9, 2022 na amekuwa kizuizini katika gereza kuu la mji wa Kinshasa, Makala.

Ndugu jamaa na marafiki wa Kabund walikuwepo mahakamani wakati wa kutolewa kwa hukumu hiyo dhidi yake. Wanachama wa chama chake wanahisi kwamba hukumu hiyo imechochewa na siasa ikitizamiwa kwamba uchaguzi mkuu unakaribia.

Uchaguzi huo umepangiwa kuandaliwa Disemba 20 na Rais Tshisekedi ambaye ameongoza DR Congo tangu Januari 2019, anawania urais akitafuta kuhudumu kwa muhula wa pili wa miaka mitano.

Share This Article