Tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 5.9 kwenye kipimo cha Richter limeshuhudiwa katikati mwa Japani leo Jumatatu ila hakuna tahadhari iliyotolewa ya uwezekano wa kutokea kwa tsunami.
Kitovu cha tetemeko hilo la saa 12:31 asubuhi ni eneo la Noto ambapo tukio sawia mwanzo wa mwaka huu lilisababisha vifo vya watu zaidi ya 230.
Maafisa wa eneo hilo walisema kwamba hakukuwa na ripoti za majeruhi ila uchunguzi ulikuwa ukiendelea.
Tetemeko la pili ambalo lilikuwa dogo kwa kipimo cha Richter lilitokea katika eneo hilo hilo leo asubuhi kulingana na mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa nchini humo.
Mwendeshaji wa mtamo wa umeme wa nyuklia wa Kashiwazaki-Kariwa ambao upo katika eneo hilo alisema kwamba wamesimamisha kazi zao ili kufanya uchunguzi wa madhara ya tetemeko hilo.