Mkewe Rais wa Uganda Janet Museveni ambaye pia ni Waziri wa Elimu nchini humo amelaani shambulizi la kigaidi lililotekelezwa katika shule ya upili ya Mpondwe Lhubiliriha, katika wilaya ya Kasese karibu na mpaka wa DR Congo.
Kulingana na Waziri huyo, shambulizi hilo la Ijumaa usiku lilisababisha vifo vya wanafunzi 37 huku wengine watano wakilazwa hospitalini.
Janet amehakikishia wananchi wa Uganda kwamba haki itatendeka.
Shule ya upili ya Mpondwe Lhubiliriha ni ya kibinafsi iliyojengwa na shirika lisilo la kiserekali linaloongozwa na Peter Hunter ambaye hufanya kazi yake nchini Uganda na Congo.
Ina mabweni mawili moja la wasichana na jingine la wavulana.
Wavulana walijifungia ndani ya bweni lao na wahalifu hao walirusha ndani bomu la petroli lililoanzisha moto na kuchoma wanafunzi 17.
Wasichana kwa upande mwingine waliamua kufungua ili watoroke lakini wahalifu wakawashambulia kwa mapanga na kuua 20 kati yao.
Usimamizi wa shirika hilo lisilo la kiserikali ulituma wakaguzi wa hesabu shuleni humo kufanya ukaguzi na waliondoka Alhamisi shambulizi likatokea Ijumaa.
Hata hivyo, Waziri amefafanua kwamba hawaambatanishi ujio wa wakaguzi hao na shambulizi bali uchunguzi unaendelea.
Anasema alitaka kuzuru shule hiyo kujionea yaliyojiri lakini bado amejitenga kwa sababu ya kutangamana na Rais Museveni ambaye ameambukizwa virusi vya korona.
Rais Museveni ametoa msaada kwa familia zilizoathirika na mkasa huo ili ziweze kuandaa mazishi ya wapendwa wao.
Waziri Janet amesihi wananchi waombee waathiriwa, wakazi wa eneo hilo wawe macho na vyombo vya habari viwajibike vinaporipoti kuhusu tukio hilo.