Jamie Foxx kuhadithia kuhusu kuugua kwake kwenye onyesho lake la Atlanta

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji, mwimbaji na mchekeshaji Eric Marlon Bishop maarufu kama Jamie Foxx, ameahidi kumwaga mtama kuhusu jinsi aliugua na kulazwa hospitalini mwaka jana kwenye onyesho lake pekee analopanga huko Atlanta.

Alitangaza hayo kupitia akaunti yake ya Instagram wiki hii wakati akitangaza onyesho hilo alilolipa mada ya “Fursa moja zaidi: Jioni moja na Jamie Foxx”.

Maneno, “Kilichofanyika ni …” nayo yanaonekana kwenye video ya tangazo la onyesho hilo ishara kwamba litakuwa onyesho la vichekesho na la kuhamasisha.

Aprili Mosi, 2023, Jamie alikimbizwa hospitalini kutokana na kile kilichosemekana kuwa tatizo la akiafya bila maelezo zaidi.

Hajawahi kusema aliugua nini lakini amekuwa akisema mara kwa mara kwamba nusura apoteze maisha akiwa hospitalini wakati huo.

Foxx atatumbuiza kwa siku tatu mfululizo Oktoba 3 hadi 5 na ametangaza kwamba atakuwa peke yake. Bado hajatangaza eneo la kuandaa onyesho hilo na hajaanza pia kuuza tiketi.

Share This Article