Jaji Mkuu Martha Koome aongoza maombolezi ya Hakimu Kivuti

Marion Bosire
1 Min Read

Jaji Mkuu Martha Koome anaongoza maafisa wa idara ya mahakama na wahusika wengine katika maombolezi ya kitaifa ya Hakimu Mkuu Monica Kivuti.

Jaji Mkuu akiwa ameandamana na wadau wa idara hiyo akiwemo mwanasheria mkuu Justin Muturi wanakutana katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi kumwomboleza mwendazake.

Kulingana na ratiba ya kikao cha mahakama ya Milimani, wageni walitarajiwa kufika saa tatu unusu asubuhi na kujaza kitabu cha rambirambi.

Padri Patric Ndung’u ataongoza maombi mafupi na kisha baadaye jumbe za maombolezi kutoka kwa wahusika wakuu. Vikao sawia vinafanyika katika vituo vyote vya mahakama kote nchini.

Hakimu Kivuti alifariki kutokana na majeraha ya risasi alizopigwa akiendelea na kazi yake katika mahakama ya Makadara Alhamisi alasiri wiki iliyopita na afisa wa polisi.

Afisa huyo naye aliuawa kwa kupigwa risasi na wenzake waliokuwa wakishika doria mahakamani.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *