Kilimo cha maparachichi kimepigwa jeki, baada ya mwekezaji mmoja kutoka Israel kuanzisha ukuzaji wa zao hilo katika shamba la ekari 400 eneo la Naivasha.
Shamba hilo kwa jina Granot International, lililoko eneo la Ndabibi, linatarajiwa kuwaajiri wafanyakazi 1,000, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka mara tatu katika miaka ijayo.
Hatua hiyo inajiri baada ya serikali ya Israel kuahidi kushirikiana na serikali ya Kenya, katika kuongeza idadi ya shamba inayotumika kwa uzalishaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Giyora Merom, alisema wataleta tajiriba yao ya miaka 70 ya ukuzaji wa maparachichi katika eneo hilo.
Giyora alitaja gharama hiyo ya ukuzaji wa zao hilo kuwa nafuu ikilinganizwa na washindani wao kutoka Peru, Chile na Uhispania.
“Tumewekeza mamilioni ya dola katika mradi huu, ambapo tunatarajia utatoa fursa kwa nafasi za ajira na soko jipya kwa zao hilo,” alisema Merom.
Balozi wa Israel hapa nchini Michael Lotem alitambua shamba hilo kuwa moja ya miradi mingi ya kilimo inayofadhiliwa na serikali ya Israel.
Alidokeza kuwa Israel kwa ushirikiano na wadau wengine, itazindua mashamba zaidi hapa nchini kwa lengo la kuwapa wakulima ujuzi.
Waziri wa kilimo kaunti ya Nakuru Leonard Bor, alisema kaunti hiyo iko makini kuongeza kiwango cha ardhi inayotumiwa kwa ukuzaji wa maparachichi.