Israel kukata rufaa dhidi ya vibali vya ICC vya kukamata viongozi wake

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wa ulinzi Yoav Gallant wanahusishwa na mashambulizi ya Gaza

Marion Bosire
1 Min Read
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu Israel

Israel imeambia mahakama ya kimataifa ya jinai ICC kwamba itakata rufaa dhidi ya vibali ilivyotoa vya kukamata waziri mkuu Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wa ulinzi Yoav Gallant.

Mahakama hiyo inalaumu wawili hao kwa matendo yao katika vita vya Gaza huku Ufaransa ikisema kwamba huenda Netanyahu akawa na kinga dhidi ya kibali cha kumkamata.

Taarifa kutoka kwa afisi ya Netanyahu jana pia iliitaka ICC kuondoa vibali hivyo vilivyotolewa kwa madai ya kutekeleza makosa ya kivita na makosa dhidi ya binadamu, kabla ya rufaa hiyo.

Wiki iliyopita, ICC ilitangaza kuwepo kwa sababu za kutosha kuhusisha Netanyahu na Gallant na hatua ya kutumia njaa kama mbinu ya kivita katika eneo la Gaza kwa kubana mawasilisho ya misaada ya kibinadamu.

Hatua ya kutaka kukata rufaa inajiri baada ya wizara ya masuala ya kigeni ya Ufaransa kusema kwamba inaamini Netanyahu anastahili kunufaika na kinga ya kukamatwa kwani Israel sio mshirika wa mahakama ya ICC.

Maoni ya Ufaransa yaliyotolewa siku moja tu baada ya kutangazwa kwa mpango wa kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah nchini Lebanon, yamekashifiwa na makundi ya kutetea haki.

Nchi nyingine kama Italia zimetilia shaka mamlaka ya Ufaransa katika kuamua hilo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *