Isongo yapatiwa walimu wapya, wavamizi waonywa

Marion Bosire
2 Min Read

Shule ya sekondari ya Mtakatifu Gabriel Isongo ilipata walimu wapya 17 waliotumwa kuhudumu huko na tume ya kuajiri walimu nchini TSC.

Hii ni baada ya walimu wa awali 17 kuhamishiwa shule nyingine kufuatia hatua ya jamii na wazazi kumfurusha mwalimu mkuu kutokana na kile walichokitaja kuwa matokeo duni.

Sasa tume ya kuajiri walimu TSC inaonya wazazi na jamii ya eneo hilo dhidi ya kuingia shuleni humo bila idhini na kuhujumu shughuli za masomo.

Mkurugenzi mtendaji wa TSC Nancy Macharia ameelezea kwamba tume hiyo inathamini sana maisha ya kila mwalimu na ndio sababu ilihamisha walimu wa awali.

Kando na kulinda maisha ya walimu hao, Macharia alisema uhamisho wao ulilenga pia kutoa fursa kwa uchunguzi wa kina kutekelezwa kuhusu kisa hicho cha uvamizi.

Wakazi wa eneo hilo na wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo walipata fursa pia kujadili suala hilo na kufahamisha TSC kuhusu hatua walizochukua za kuhakikisha usalama wa walimu.

Walimu wapya 17 waliotumwa kuhudumu kwenye shule hiyo ya St. Gabriel Isongo wanahitajika kuripoti kazini mara moja ili shughuli za masomo ziendelee.

Macharia anasema wameanzisha mpango mpya wa kutathmini utendakazi wa walimu ili kuhakikisha matokeo mazuri na kuchukua hatua dhidi ya walimu ambao utendakazi wao utakosa kuafiki viwango.

Macharia alisema haya Jumanne baada ya kukutana na wabunge wa eneo la Magharibi mwa nchi hasa kaunti ya Kakamega ambako shule hiyo iko.

Share This Article