Isaac Mutuma aapishwa kuwa Gavana wa Meru

Hii ni baada ya mahakama kuu kudumisha uamuzi wa bunge la Seneti wa kumwondoa madarakani Gavana Kawira Mwangaza.

Marion Bosire
2 Min Read
Isaac Mutuma (alivevalishwa maua) wakati wa kuapishwa kuwa Gavana wa kaunti ya Meru

Naibu Gavana wa kaunti ya Meru Isaac Mutuma ameaapishwa leo Jumatatu, majira ya saa 4:15 asubuhi kuwa Gavana wa nne wa kaunti ya Meru. 

Hafla ya kuapishwa kwake iliandaliwa katika uwanja wa Mwendantu mjini Meru na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kaunti hiyo akiwemo Gavana wa zamani Kiraitu Murungi na Seneta wa zamani Mithika Linturi.

Seneta wa sasa wa kaunti ya Meru Kathuri Murungi pia alikuwa miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo.

Uapisho wa naibu Gavana huyo, unafuatia uamuzi wa mahakama kuu wa kudumisha kuondolewa madarakani kwa Gavana Kawira Mwangaza mnamo siku ya Ijumaa, tarehe 14 mwezi Machi mwaka jana.

Mwangaza alikuwa ameponea majaribio mawili ya kumbandua mamlakani awali, moja likiwa la Disemba mwaka 2022 ambapo kamati ya bunge la Seneti ilitupilia mbali madai dhidi yake.

Jaribio la pili lilijiri Novemba 2023, ambapo suala hilo lilijadiliwa na bunge zima la Seneti na akaponea baada ya kuomba msamaha.

Mara ya tatu na ya mwisho, bunge la Seneti lilikubaliana na bunge la kaunti ya Meru mwezi Agosti mwaka 2024 na kumwondoa afisini kwa makosa mbalimbali.

Usalama uliimarishwa maradufu wakati wa uapisho huo uliohudhuria na wakazi wengi wa kaunti ya Meru.

Kubanduliwa kwa Gavana Mwangaza kunamaanisha kuwa idadi ya Magavana wanawake imepungua kutoka saba hadi sita.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *