Iran yakanusha madai ya adhabu kali dhidi ya Ronaldo

Marion Bosire
1 Min Read

Ubalozi wa Iran nchini Uhispania umekanusha madai kwamba mchezaji soka wa kimataifa Cristiano Ronaldo amehukumiwa adhabu ya viboko 99 nchini Iran.

Taarifa zilisambaa kwamba mawakili kadhaa wa Iran walikuwa wamekwenda mahakamani nchini Iran kumshtaki Ronaldo baada yake kukumbatia na kubusu mchoraji wa kike wa Iran.

Uvumi ulitaja hatua yake kuwa kosa la uzinzi ambalo adhabu yake ni viboko 99. Wanaume katika taifa la Iran hawaruhusiwi kugusa kwa vyovyote wanawake ambao hawajaolewa.

Kulingana na ubalozi huo jijini Madrid, hakuna adhabu yoyote imetolewa nchini Iran dhidi ya mwanasoka yeyote wa kimataifa.

Kupitia taarifa ubalozi huo ulishangaa jinsi habari kama hizo za uwongo zimepatiwa kipaumbele huku watu wakisahau uhalifu dhidi ya binadamu unaotekelezwa huko Palestina.

Taarifa hiyo ilifafanua kwamba video inayosambazwa inayoonyesha Ronaldo akimkumbatia na kumbusu Bi. Fatemeh Hamami ambaye ni mchoraji wa kike mlemavu sio ya sasa bali ni ya Septemba wakati Ronaldo alisafiri hadi Iran kwa ajili ya mchuano.

“Mkutano wake wa kikweli na kiutu na Fatemeh Hamami ulisifiwa pia na wananchi wa Iran na usimamizi wa michezo nchini Iran.” ilisema taarifa hiyo ya ubalozi.

Share This Article