Afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ODPP, imeagiza halmashauri ya kutathmini utendakazi wa polisi,IPOA, kuchunguza na kuwasilisha ripoti kuhusu mauaji ya Rex Masai ndani ya siku 21.
Kupitia kwa taarifa, afisi hiyo iliitaka IPOA kuchunguza mauaji hayo yaliyotekelezwa Alhamisi jioni kwa makini na kikamilifu.
“Kwa mujibu wa sehemu ya 157(4) ya katiba ya Kenya, Mkurugenzi wa mashtaka ya umma ameagiza halmashauri ya kutathmini utendakazi wa polisi (IPOA), kuchunguza kikamilifu swala hilo na kuwasilisha matokeo ndani ya siku 21,” ilisema taarifa hiyo.
Hapo awali IPOA ilisema imeanzisha uchunguzi kufuatia mauaji hayo ya Rex Masai na mtu anayedaiwa kuwa afisa wa polisi.
Rex alipigwa risasi Alhamisi jioni wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha 2024 jijini Nairobi.
Mswada huo ulipitishwa bungeni baada ya kusomwa kwa mara ya pili ambapo wabunge 204 waliunga mkono mswada huo, huku wabunge 115 wakiupinga.