Mamlaka Huru ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi nchini, IPOA inasema inachunguza jumla ya vifo 39 na watu 150 waliojeruhiwa vibaya wakati wa mandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 wiki mbili zilizopita.
Idadi hiyo ya vifo inaonekana kuwiana na ile iliyotolewa na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu nchini, KNCHR iliyosema katika uchunguzi wake wa awali kwamba imebaini kuwa watu 39 walifariki wakati wa maandamano hayo.
Utawala wa Kenya Kwanza umeonekana kuashiria kuwa watu 19 walifariki wakati wa maandamano hayo.
Katika taarifa, mwenyekiti wa mamlaka hiyo Anne Makori anasema wamepiga hatua katika kuchunguza kilichosababisha vifo vya Rex Kanyike Masai, Evans Kiraitu na vifo vya jumla ya watu 11 vilivyothibitishwa kutokea jijini Nairobi ikiwa ni pamoja na katika majengo ya bunge Juni 25, 2024.
Masai alidaiwa kupigwa risasi na kuuawa na afisa wa polisi aliyevalia nguo za kiraia Juni 20, 2024 jijini Nairobi na kuibuka kuwa kifo cha kwanza kuripotiwa tangu kuanza kwa maandamano hayo. IPOA inasema imepiga hatua katika kubaini chanzo cha kifo chake ikiwa ni pamoja na kuandikisha taarifa za mashuhuda na kushiriki shughuli ya upasuaji wa mwili wake. Inasema kilichosalia ni kusubiri ripoti za wataalam na kuandikisha taarifa kutoka kwa watu zaidi walioshuhudia akiuawa.
Mtaani Githurai kulikodaiwa kufanyika ufyatuaji risasi Juni 25, 2024 usiku, IPOA inasema imeanzisha uchunguzi kuhusiana na kifo cha Andrew Mwawasi na mtoto mwenye umri wa miaka 5 kwa jina Gianna Merkel Obonyo aliyebainika kupigwa risasi kifuani. Mtoto huyo alitibiwa katika hospitali ya rufaa ya Kenyatta, KNH na baadaye kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Kifo kingine kinachochunguzwa na IPOA ni kile cha mtoto mwenye umri wa miaka 12 kwa jina Master Kennedy Onyango aliyedaiwa kufariki baada ya kumiminiwa risasi mtaani Ongata Rongai katika kaunti ya Kajiado. Mwili wa mwenda zake tayari umefanyiwa upasuaji na kubainika kwamba alifariki kutokana na majeraha ya risasi.
Mamlaka hiyo sasa inatoa wito kwa Wakenya ambao huenda walishuhudia visa vya waathiriwa kupigwa risasi kuwasiliana nayo ili kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuharakisha uchunguzi unaoendelea kufanyika.
Kulingana na IPOA, imebaini kuwa jumla ya watu 7 walitekwa nyara wakati wa maandamano hayo.
Inasema kukamatwa na kushtakiwa kwa maafisa wa polisi waliohusika katika ufyatuaji risasi huo kutafanyika punde baada ya kubaini ukweli wa mambo na faili za maafisa husika kukabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP. Uamuzi wa ama kuwashtaki maafisa hao au la uko mikononi mwa DPP.