Serikali imetangaza kesho Ijumaa, Novemba 1, 2024 kuwa sikukuu ya taifa.
Kupitia kwa gazeti rasmi la serikali, Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, alisema hatua hiyo ni kutokana na kuapishwa kwa Prof. Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais wa taifa.
“Kuambatana na sehemu ya 3 kuhusu sheria za siku kuu za umma, Ijumaa Novemba 1,2024 imetangzwa kuwa siku kuu ya taifa, ikiwa ni siku ya kuapishwa kwa Naibu rais mteule,” ilisema sehemu ya gazeti rasmi la serikali.
Kindiki ataapishwa siku moja baada ya Mahakama Kuu kuondolea mbali maagizo ya kuzuia kuapishwa kwake yaliyokabidhiwa mtangulizi wake Rigathi Gachagua aliyeondolewa katika wadhifa huo.
Kindiki ataapishwa Ijumaa kuwa Naibu Rais, katika sherehe itakayoandaliwa katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa, KICC, kati ya saa nne asubuhi na saa sita adhuhuri.