Mkurugenzi wa idara ya utabiri wa hali ya hewa hapa nchini David Gikungu, ameomba msamaha kutokana na mkanganyiko wa mawasiliano kuhusu mvua za El Nino.
“Ningependa kudokeza kuwa, jinsi ilivyoelezewa hapo awali tunashuhudia mvua za El Nino wakati huu wa mvua za vuli. Hata hivyo tunaomba radhi kwa kukosa kuwasiliana kwa kuwa hatua hiyo ni kosa kubwa,”alisema Gikungu.
Gikungu alisema taifa hili linapaswa kuendelea kujitayarisha kutokana na mvua kubwa inayosababishwa na hali ya El Nino.
Hatua ya kuomba radhi ya Mkurugenzi huyo, inajiri baada ya hotuba ya naibu Rais Rigathi Gachagua kwa taifa, akielezea hatua za serikali za kukabiliana na uharibufu wa Mali na kupoteza kwa maisha.
Hapo awali Rais William Ruto alidokeza kuwa taifa hili halitashuhudia mvua za El Nino jinsi ilivyokuwa imetabiriwa hapo awali.
Gachagua alitambua madhara makubwa ambayo yamesababishwa na mvua, huku kaunti 19 zikiathirika zaidi.
Serikali pamoja na washirika wengine inajizatiti kutoa misaada katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko kote nchini.