Idara ya Mahakama imesitisha kimya chake na kujiunga na wanaolaani visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara humu nchini.
Kumekuwa na ripoti za watu wasiopungua watatu, hasa vijana wanaodhaniwa kuwa wakosoaji wa serikali kutekwa nyara katika siku za hivi karibuni, na kuibua kumbukumbu ya hali ilivyokuwa wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z miezi michache iliyopita.
Kwenye taarifa, Idara ya Mahakama inayoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome imelaani kuchipuka tena kwa visa vya utekaji nyara ikivitaja kuwa ukiukaji wa sheria.
“Idara ya Mahakama imepata kufahamu ripoti za hivi karibuni za kuibuka tena kwa visa vya utekaji nyara. Kenya ni nchi ya kidemokrasia inayoongozwa na katiba, ambapo utawala wa sheria unasimama kama maadili ya msingi na kanuni elekezi ya maongozi yetu,” imesema Idara ya Mahakama.
“Utekaji nyara hauna nafasi katika sheria na ni tishio la moja kwa moja kwa haki za raia.”
Kufuatia kuibuka kwa ripoti hizo, Idara ya Mahakama inatoa wito kwa asasi za usalama na taasisi husika kutii sheria ili kulinda haki na uhuru wa raia.
Idara hiyo imeyasema hayo wakati ambapo Huduma ya Taifa ya Polisi nchini, NPS imekanusha madai kwamba maafisa wa polisi wanahusika katika visa vya utekaji nyara vinavyoshuhudiwa nchini kwa sasa.
Kwenye taarifa leo Alhamisi, Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja ameelezea kutoridhishwa na taarifa zinazosambazwa zikiwatuhumu maafisa wa polisi kwa utekaji nyara huo akizitaja kuwa za uongo.
Kanja anasema mamlaka ya maafisa wa polisi yanahusu tu kuwakamata wanaovunja sheria kwa njia inayokubalika na wala sio kuwateka nyara.
“Mchakato kulingana na sheria za huduma uko wazi: shughuli zote za kukamata wahalifu lazima zinakiliwe kwenye kitabu cha matukio ili wafikishwe mahakamani baadaye,” alielezea Kanja kwenye taarifa yake.
Amesema iwapo mtu hatafikishwa mahakamani basi anafaa kuachiliwa huru.
Aidha, amebainisha kuwa hakuna mtu yeyote aliyetekwa nyara anazuiliwa katika kituo chochote cha polisi kote nchini.
Mamlaka ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi, IPOA tayari imesema inachunguza visa vya hivi punde vya utekaji nyara.
Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga sawia na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ni miongoni mwa viongozi ambao wameshutumu vikali ripoti za kurejea kwa visa vya utekaji nyara nchini.
Raila ametaja utekaji nyara huo kuwa mbinu ya zamani iliyopitwa na wakati na isiyokubalika kisheria.