Idara ya Mahakama inakusudia kufanya marekebisho muhimu katika mfumo wa idara hiyo ili kukabiliana na msongamano wa wafungwa katika magereza humu nchini.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kukuza urekebishaji mwafaka wa tabia miongoni mwa wafungwa.
Jaji Mkuu Martha Koome amesema idara ya mahakama itapigia debe matumizi ya Maagizo ya Kutumikia Jamii (CSOs) kwa kupitia upya hukumu, na panapostahili, kuwaachilia huru wafungwa kuhudumia jamii badala ya kutumikia vifungo.
Koome amesema marekebisho hayo yanajumuisha juhudi za haraka na endelevu za kubadilisha idara ya magereza na kuifanya kuwa ile inayoakisi viwango vya juu vya haki na heshima kwa binadamu.
“Mpango wa Matokeo ya Haraka umeratibiwa kwa lengo kuu la kuafikia idadi inayoweza kudhibitiwa ya wafungwa inayowiana na uwezo uliowekwa wa magereza yetu. Hali ya sasa ya magereza haidhibitiki,” alisema Koome.
Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango wa upunguzaji wafungwa katika gereza la Industrial Area jijini Nairobi.
Kulingana na Koome, awamu ya kwanza ya mpango huo inatilia mkazo upitiaji upya wa dhamana za wafungwa walioko katika magereza katika eneo la Nairobi.