Katika hatua ya kukabiliana na ufisadi katika idara ya mahakama, Jaji Mkuu Martha Koome amezindua mkakati mpya inayohusisha ujasusi kwa kushirikiana na tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC na huduma ya kitaifa ya ujasusi NIS.
Tangazo hili lilitolewa katika uzinduzi wa njia ya mtandao wa kongamano la kila mwaka la mahakama ya hakimu na ile ya Kadhi huko Naivasha.
Koome alisisitiza kwamba idara ya mahakama sasa inatumia mbinu makinifu ya kutambua maeneo ya ufisadi na wanaohusika na matendo yaliyo kinyume na maadili kabla hayajaongezeka.
Mabadiliko haya ni hatua kubwa kutoka mbinu za awali ambapo juhudi zilitegemea tu malalamishi yaliyowasilishwa kwa tume ya huduma za mahakama na ile ya haki ya kiutawala.
“Tumejitolea kuunda eneo lisilo na ufisadi katika idara ya mahakama” alisema Koome huku akisisitiza sera ya idara hiyo ya kutovumilia kabisa ufisadi.
Jaji mkuu alitambulisha pia kamati za uadilifu katika mahakama ambazo zitakuwa majukwaa ya maafisa wa idara ya mahakama, wawakilishi wa EACC na wadau wengine kushirikiana kushughulikia utovu wa maadili.
Alihimiza kukumbatiwa kwa vifaa vya kidijitali kama uwasilishaji kesi kidijitali na vikao vya mitandaoi vya mahakama ili kuimarisha utoaji huduma.
“Teknolojia itakuwa nguzo muhimu katika kubadili idara ya mahakama na kushughulikia kucheleweshwa kwa utatuzi wa kesi.” aliongeza Koome huku akipongeza vituo vya mahakama vilivyo na idadi ndogo ya uahirishaji wa kesi.