Jaji Mkuu Martha Koome, ameelezea wasiwasi kuhusu ukosefu wa fedha za kutosha katika idara ya mahakama, akidokeza kuwa haipatiwi umuhimu mkubwa ikilinganishwa na idara zingine kama vile elimu, afya na usalama wa taifa.
Koome, ambaye ni Rais wa Mahakama ya Upeo ya Kenya, alisisitiza kuwa idara ya Mahakama inapaswa kupokea mgao sawa wa bajeti na idara zingine za serikali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mahakama ya Kamwangi katika eneo la Gatundu Kaskazini, kaunti ya Kiambu, Jaji huyo Mkuu alisema uhaba wa fedha umehujumu uwezo wa idara ya Mahakama kuwaajiri Majaji, Mahakimu na wafanyakazi wengine ili kuhakikisha utekelezaji wa haki kikamilifu.
“Tunapaswa kushughulikia upatikanaji wa haki sawa na ilivyo katika sekta ya Afya, Elimu na Usalama wa taifa. Hatuwezi zungumzia mrundiko wa kesi wakati tunakabiliwa na uhaba wa fedha,” alisema Koome.
Wakati huo huo Koome, alisema kuwa licha ya changamoto za kifedha, mrundiko wa kesi umepungua kwa asilimia 2.16 kutoka kesi 649, 342 hadi 635, 262 katika kipindi cha mwaka 2023/2024.
Alisema idara hiyo inalenga kufungua mahakama katika maeneo bunge yote 290. Hadi kufikia sasa Koome alisema mahakama 141 zimekamilika, huku akitoa wito kwa wabunge katika maeneo bunge 149 yaliyosalia kushirikiana na afisi yake kufanikisha mpango huo.