Idara ya magereza yatakiwa kupiga jeki usalama wa chakula nchini

Tom Mathinji
1 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa idara ya magereza kutumia taasisi zake kuhakikisha usalama wa chakula hapa nchini.

Gachagua alisema idara hiyo ina uwezo mkubwa wa kujitosheleza kwa chakula kwa kuwa inamiliki mashamba makubwa.

“Hakuna sababu kwanini idara ya magereza haiwezi zalisha chakula cha kutosha kwa wafungwa, badala ya kununua chakula. Idara za urekebishaji tabia zina ardhi kubwa sana,” alisema Gachagua.

Naibu huyo wa Rais aliyasema hayo siku ya Jumatano katika jumba la mikutano ya kimataifa KICC, baada ya kuzindua wiki ya urekebishaji tabia.

Huku akipongeza idara hiyo kwa kubadilisha maisha ya wafungwa, kuwarekebisha tabia na kuwarejesha tena katika jamii, Gachagua aliwahimiza maafisa wa magereza kujihusisha na upanzi wa miti, huku taifa hili likilenga kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.

“Wajibu wetu sio tu kurekebisha tabia, mbali pia kulinda mazingira. Maswala tunayopaswa kuzingatia ni pamoja na kukuza miche katika vituo vyetu vya urekebishaji tabia,” aliongeza Naibu huyo wa Rais.

Naibu Rais alikuwa ameandamana na katibu katika idara ya magereza Salome Muhia-Beacco, Kamishna mkuu wa magereza Brigedia mstaafu John Kibaso Warioba, Seneta wa Nandi Samson Cherargei, miongoni mwa wengine.

Share This Article