Idadi ya wanawake wanaojitosa katika siasa nchini imeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Tume huru ya Uchaguzi na mipaka nchini (IEBC) imetoa taarifa hiyo huku ikiongeza kuwa licha ya idadi ya wanawake waliochaguliwa kwenye nyadhfa za uongozi kuimarika, bado idadi hiyo ni ndogo na ipo haja ya kutoa uhamasisho zaidi.
Afisi Mkuu mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan, amesema wanawake wakihamasishwa kuhusu mchakato wa uchaguzi upo uwezekano wa idadi hiyo kuongezeka ifikiapo uchaguzi wa mwaka 2027.
Kulingana na Hussein wanapanga kuwasilisha mswada bungeni kushurutisha vyama vya kisiasa kutanguliza jina la wagombea wa kike na wala sio la wa kiume, ilivyo desturi.
IEBC inasema hili litaongeza idadi ya wanawake wanaoshiriki uchaguzi na hata kuimarisha idadi yao bungeni.
Ametaja baadhi ya mikakati iliyowekwa na tume hiyo ili kuimarisha idadi ya wanawake wanaoshiriki uchaguzi ikiwemo kupunguza ada ya uteuzi kwa wanawake wanaogombea nafasi za uchaguzi, kutoidhinisha orodha ya wagombeaji uchaguzi ya vyama vya kisiasa vinavyokiuka sheria ya thuluthi mbili, pamoja na kuhakikisha wanawake wengi wanashirikishwa katika maswala ya uchaguzi
Hata hivyo idadi ya wanawake waliochaguliwa kwenye nyadhfa za uongozi nchini mwaka wa 2022 iliongezeka ikilinganishwa na ile ya mwaka wa 2022 ambapo wabunge wanawake 30 walichaguliwa na waakilishi wadi 114 mwaka wa 2022, ikilinganishwa na wabunge 23 na MCA’S 96 waliochaguliwa mwaka wa 2017.
Richard Chalagat afisa wa fedha katika shirika la wanawake wasomi wa Afrika (FAWE) amefichua kuwa ipo haja ya kuwahamasisha wanawake kuhusu mchakato wa uongozi pamoja na uchaguzi wakiwa na umri mdogo.
Upande wao walemavu wamesema vyama vikuu vya kisiasa vinawatenga wakati wa zoezi la mchujo hali inayowatamausha kujitosa katika siasa na kushiriki uchaguzi.
Haya yalijiri katika hafla ya shirika la FAWE iliyoandaliwa katika kaunti ya Machakos.