Idadi ya watu waliofariki kutokana na maandamano ya upinzani dhidi ya serikali imefikia 17, baada ya mili mingine minne kupatikana katika kaunti ya Nairobi.
Kulingana na ripoti ya polisi, miongoni mwa walioangamia ni bingwa wa mashindano ya ndondi ya Nairobi Open katika uzani wa Bantam Raphael Shigali aliyejipata na majeraha ya risasi na alijipata katika kundi la watu waliokuwa wakitoroka polisi mtaani Hamza alipofyatuliwa risasi.
Mtu mmoja pia ameripotiwa kufariki katika mtaa wa Mukuru, alipogongwa na mkebe wa kitoa machozi kifuani akitoka katika kituo kimoja cha afya.
Mtaani Majengo, wakazi walipeleka mwili wa mwanamume mmoja katika kituo cha polisi huku mwili huo ukiwa na majeraha ya kudungwa kisu.
Watu wengine wawili zaidi wameripotiwa kufariki kaunti ya Kisumu kutokana na maandamano.
Haya yanajiri huku serikali ikianzisha uchunguzi wa kina na kuwatia mbaroni washukiwa wakuu wa maandamano ya juzi Jumatano.
Upinzani sasa unasema utaandaa maandamano hayo kwa siku tatu mtawalia kuanzia Jumatano wiki ijayo.