Idadi ya watu walioangamia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyoandamana na kimbunga mjini Derna nchini Libya imegonga 5,200 huku wengine 5,000 wakiwa hawajulikani waliko na zaidi ya 7,000 wakiuguza majeraha.
Mvua hiyo kubwa iliyoandamana na kimbunga kijulikanacho kama Daniel, ilisababisha mabwawa mawili kuvunjika na kusababisha maafa makubwa kwa kusomba majengo na watu Jumapili jioni.
Mji wa Derna ulio karibu na bahari ya Mediterranean una wakaazi 100,000 huku shirikisho la kimataifa la msalaba mwekundu likiripoti kuwa huenda idadi ya maafa ikaongezeka zaidi .

Shughuli za kutafuta mili zinaendelea huku matumaini ya kupata manusura zaidi yakididimia na inakisiwa kuwa takriban watu 60,000 wameachwa bila makao wengi wakiwa kwenye kambi .
Yamkini mabwawa hayo hayajafanyiwa ukarabati tangu mwaka 2002 na moja wapo ya bwawa lilikuwa na kina cha mita 230 na ndilo lilipasuka baada ya kujaa maji kabla bwawa la pili pia kupasuka na maji yote kuelekea katika mji wa Derna yakisomba kila kitu.