Ichung’wah: Wenyekiti wa kamati za bunge wasiohudhuria vikao kufurushwa

Martin Mwanje
2 Min Read

Wenyekiti wa kamati za bunge na manaibu wao walio na mazoea ya kutohudhuria vikao vya bunge wanakabiliwa na hatari ya kubanduliwa kwenye nyadhifa hizo. 

Onyo hilo limetolewa na kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah.

Matamshi yanakuja wakati kufuatia kukosekana kwa wabunge ambao maswali yao yaliratibiwa kujibiwa na Waziri wa Uchukuzi na Barabara Davis Chirchir.

Ichung’wah amesisitiza kuwa bunge halipaswi kukabiliwa na tatizo la ukosefu wa idadi ya kutosha ya wabunge ili kuendesha vikao vyake.

Hii ni ikizingatiwa kwamba kuna zaidi ya wenyekiti wa kamati za bunge zaidi ya 60 na manaibu wao ambao uwepo wao utawezesha shughuli za bunge kuendelea kama kawaida.

Kifungu Namba 121 cha Katiba kinahitaji uwepo wa wabunge wasiopungua 50 katika Bunge la Taifa ili kuendesha shughuli zake wakati Maseneta 15 wakihitajika katika Bunge la Seneti.

Ichung’wah ambaye pia ni mbunge wa eneo bunge la Kikuyu anasema ikiwa kutakuwa na uongozi madhubuti, Bunge la Taifa lina wenyekiti wa kamati za bunge na manaibu wao wa kutosha kukidhi mahitaji hayo ya katiba.

Bunge la Taifa limerejelea vikao vyake baada ya kwenda mapuzikoni kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Hata hivyo, Naibu Spika Gladys Shollei jana Jumatano alilazimika kuagiza kupigwa kwa kengele baada ya kugundulika kuwa kulikuwa na chini ya wabunge 50 bungeni.

“Tulikuwa katika mkutano wa uongozi wiki jana ulioongozwa na Spika na Tume ya Huduma za Bunge, ambako washiriki walielezea mashaka juu ya idadi ya wabunge wanaohudhuria vikao vya bunge, hasa wenyekiti wa kamati na manaibu wao,” alilalamika Ichung’wah.

“Bunge hili lina wenyekiti wasiopugua 60 wa kamati za bunge. Tunahitaji tu wabunge 50 kuendesha shughuli za bunge.”

 

Share This Article