Kinara wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah amejibu waraka wa mwaliko kwa meza ya mazungumzo kutoka kwa upinzani.
Kiongozi wa muungano wa Azimio katika mazungumzo hayo Kalonzo Musyoka alinukuliwa akisema jana Alhamisi kuwa alikuwa amewaalika wanachama wa serikali kwa mazungumzo katika hoteli ya Serena kuanzia Jumatatu, Agosti 8 kuanzia saa tano asubuhi .
Kiongozi huyo wa wengi amekiri pia wako tayari kwa mazungumzo hayo, huku akitumai yataharakishwa na kukamilika kabla ya mwishoni mwa mwezi huu.
Kando la Kalonzo, wanachama wengine wa timu ya upinzani ni kiongozi wa wachache katika bunge la taifa Opiyo Wandayi, Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni, mbunge wa Malindi Amina Mnyanzi na Waziri wa zamani wa Ulinzi Eugene Wamalwa.
Kwa upande mwingine, Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot, Gavana wa Embu Cecily Mbarire, Mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Bungoma Catherine Wambilianga na mbunge wa EALA Hassan Omar watajumuika na Ichung’wah kuuwakilisha utawala wa Kenya Kwanza.
Kuteuliwa kwa wanachama wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, uwekwaji wa sheria ya jinsia na Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge, CDF ni miongoni mwa masuala yanayotarajiwa kujadiliwa wakati wa mazungumzo hayo.
Hata hivyo, haijabainika ikiwa suala la gharama la maisha litaangaziwa kwani pande zote mbili zina mitazamo kinzani kulihusu.