Huzuni imetanda katika mji wa Gatundia, Kaunti ya Laikipia kufuatia mauaji ya ajuza mmoja, uovu uliotekelezwa na watu wasiojulikana.
Lucy Wanjiru Ndungu alivutwa kutoka dukani kwake hadi jikoni ambapo alipigwa shingo kwa kisu na kuchinjwa kwa panga, kwa mujibu wa majirani.
Washukiwa walitumia fursa ya wengi wa wakazi kuwa kanisani kumshambulia mwanamke huyo aliyekuwa peke yake nyumbani.
Mumewe, Wilson Ndungu ambaye alikuwa akichunga mifugo ya familia upande mmoja wa shamba, alishtuka alipoona madoadoa ya damu nje ya nyumba alipokwenda nyumbani kuchukua maji.
Alilia kwa mshtuko alipogundua mwili wa mkewe ukiwa chini ukiwa umejaa damu jikoni. Karibu na mwili kulikuwa na kisu cha jikoni na panga vinavyoaminika kuwa silaha za mauaji.
Maafisa wa upelelezi wa jinai DCI walifika katika eneo la tukio na kutekeleza uchunguzi wao. Walichukua silaha hizo na sampui nyingine.
Wauaji wanaaminika kushambulia mama huyo akiwa kweye stoo kuchukua viazi kwa ajili ya chakula cha mchana kwani viazi vilikuwa vimetapakaa nje ya duka, kulingana na jirani mmoja.
Familia ya marehemu inaishi katika mashamba makubwa eneo lililo mbali kidogo na mji wa Gatundia.
Mume wake aliyekumbwa na mshtuko hangeweza kusema lolote na alikaa akitazama watu waliokuwa wakizunguka nyumbani.
Majirani walisema hivi maajuzi mbuzi wa maziwa aliibwa kutoka nyumbani.
Polisi walichukua mwili na kuupeleka kwenye hifadhi ya maiti ya hospitali ya Kaunti ya Nyahururu.