Huduma ya taifa ya misitu KFS imetoa maelekezo kuhusu kulisha mifugo katika misitu ya serikali kote nchini.
Kwenye taarifa kwa vyumba vya habari ya Juni, 10, 2024, huduma ya taifa ya misitu imeelezea kwamba mtunzaji mkuu wa misitu ametoa maelekezo hayo kwa misingi ya sheria ya mwaka 2016 kuhusu usimamizi na utunzaji wa misitu nchini.
Sheria hiyo inakubalia makundi yaliyosajiliwa ya jamii zinazoishi karibu na misitu kushiriki katika utunzaji wa misitu huku zikunufaika na misitu hiyo.
Malisho kwa mifugo ni mojawapo ya manufaa jamii hizo hupata ndiposa maelekezo ya matumizi ya misitu kwa kulisha mifugo yametolewa.
Mtunzi mkuu wa misitu amesema kwamba maeneo mwafaka ya kulisha mifugo yatatengwa katika misitu na kwamba jamii hizo hazitakubaliwa kulisha mifugo katika maeneo ya mashamba makubwa na maeneo muhimu kiikolojiakama maeneo chepechepe na chemichemi za maji.
Kila eneo la kulisha mifugo litakuwa na sajili inayoonyesha jina la eneo, jina la kila mfugaji, nambari yake ya kitambulisho na idadi na aina ya mifugo wake na idadi ya mifugo wanaopaswa kulishwa katika kila eneo itawekwa na msimamizi wa eneo husika.
Wafugaji wote watahitajika kupata kibali cha kulisha mifugo wao kwenye msitu kila mwezi na hakuna mifugo watakubaliwa kuwa katika maeneo hayo ya malisho usiku kati ya saa moja jioni na saa moja asubuhi.
Mfugaji ambaye atakiuka maelekezo mapya atapoteza haki ya kulisha mifugo wake kwenye msitu, ashtakiwe au adhabu zote mbili kwa pamoja huku mifugo waliotelekezwa katika maeneo husika wakitwaliwa naserikali.