Hospitali zatakiwa kuwahudumia wagonjwa chini ya SHA

Martin Mwanje
1 Min Read

Hospitali zote nchini zimetakiwa kuhakikisha wanachama wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) wanaendelea kupata huduma za matibabu kama kawaida. 

Katibu wa Idara ya Huduma za Matibabu Harry Kimtai ameelezea kujitolea kwa serikali kuzisaidia hospitali kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa bila matatizo yoyote wakati huu wa mpito.

Bima mpya ya Afya ya Jamii (SHIF) ilizinduliwa jana Jumanne kote nchini.

“Serikali impeokea vyema mwitikio chanya wa hospitali, huku hospitali nyingi tayari zikitia saini mikataba chini ya vifungu vya utoaji huduma vya (HCP) vya SHA,” amesema Kimtai katika taarifa.

“Hospitali zinatakiwa kuendelea kutoa huduma kwa mujibu wa mikataba hii, zikihakikisha hakuna mgonjwa yeyote atakayefukuzwa na kwamba huduma muhimu kama vile matibabu ya figo, saratani na huduma kwa kina mama wanaojifungua zinapatikana kikamilifu.”

Wizara ya Afya inasema inafanya kila iwezalo kuhakikisha inakuza uelewa wa umma kuhusiana na bima mpya ya afya ya SHIF kupitia mitandao ya kijamii na tovuti ya SHA.

Ripoti zinaashiria kuwa Wakenya wengi wamechanganyikiwa kuhusiana na bima hiyo huku wengi wakiwa hawafahamu namna ya kujisajili na manufaa ya bima hiyo.

Share This Article