Waziri mpya wa Afya Aden Duale ameahidi kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) inalipa fedha zote inazodaiwa na hospitali tarehe 14 kila mwezi.
Duale, aliyezungumza wakati akichukua hatamu za uongozi wa wizara hiyo kutoka kwa mtangulizi wake Dkt Deborah Barasa leo Jumanne, ametaja mpango huo, almaarufu TaifaCare, uliozunduliwa Oktoba 1, 2024 kuwa muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa afya kwa wote kote nchini.
“Ni moja ya mipango yenye kuleta mabadiliko zaidi katika historia ya nchi yetu, ukiwa umejikita kwa usawa, umoja na imani kwamba hakuna Mkenya anapaswa kufariki kwa sababu ya kukosa huduma bora za matibabu,” alisema Duale wakati wa hafla hiyo.
Kulingana naye, jumla ya Wakenya milioni 20.8 wamejiandikisha kwa SHA pamoja na jamaa wao milioni 5.7.
Kaunti ambazo zinaongoza katika uandikishaji wa SHA ni Mombasa, Bomet, Nyeri, Elgeyo Marakwet na Kirinyaga.
Waziri Duale ametoa wito kwa kaunti zingine kuiga mfano huo na kuongeza kasi ya uandikishaji wa wakazi kwa mpango wa SHA.
Kulingana na Waziri huyo, jumla ya shilingi bilioni 25.4 zimelipwa na SHA kwa hospitali zinazotoa huduma chini ya mpango huo.
Ahadi ya Duale inakuja wakati ambapo hospitali mbalimbali zimekuwa zikiisuta SHA kwa kuchelewa kulipa malimbikizi ya fedha zake katika hatua ambayo imesababisha hospitali za kibinafsi kusitisha utoaji huduma.