Homa Bay yazindua kituo cha ukusanyaji wa taarifa za tabia nchi

Martin Mwanje
1 Min Read

Serikali ya kaunti ya Homa Bay imezindua kituo chake cha kukusanya taarifa kuhusiana na tabia nchi.

Gavana Gladys Wanga aliongoza hafla ya uzinduzi wa kituo hicho katika Ofisi za Idara ya Nishati, Misitu na Mabadiliko ya Tabia Nchi katika kaunti hiyo leo Alhamisi.

Kitatumiwa kukusanya, kuchambua, kutayarisha na kusambaza taarifa zinazohusu tabia nchi kama vile halijoto, mvua, upepo, unyevu wa udongo na hali za ziwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Gavana Wanga alisema taarifa zitakazokusanywa zitakuwa muhimu kwa wakulima katika kaunti hiyo kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao za kilimo.

Aliongeza kuwa zitakuwa zenye manufaa kwa watekeleza na watunga sera katika kaunti hiyo ikizingatiwa pia kitatumiwa kupokea simu zitakazosaidia katika usimamizi wa majanga.

“Taarifa tutakazotoa kwa wakulima na wavuvi wetu zitakuwa muhimu kwao katika kuwawezesha kuweka mipango sahihi na kutekeleza shughuli zao za kilimo,” alisema Gavana Wanga.

Sera ya Mabadiliko ya Tabia Nchi ya Kaunti ya Homa Bay ya mwaka 2022 inapendekeza matumizi ya sera stahiki kwa ukusanyaji wa kutegemewa, uchambuzi na usambazaji wa taarifa za tabia nchi.

Wakulima na raia kwa jumla wanaweza wakatumia nambari isiyotozwa malipo ya 0800000870 kuwasiliana na kituo hicho.

Share This Article