Hoja ya kumbandua Gachagua: Vikao vya kukusanya maoni kuendelea kwa siku moja zaidi

Tom Mathinji
2 Min Read
Vikao vya bunge

Bunge la kitaifa limeongeza siku moja zaidi kwa vikao vinavyoendelea vya ushirikishwaji umma kuhusu kung’atuliwa mamlakani kwa naibu rais Rigathi Gachagua.

Kupitia kwa taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa X,  karani wa bunge la kitaifa Samuel Njoroge, alisema shughuli hiyo ambayo iliratibiwa kukamilika leo sasa itakamilika kesho.

“Zoezi la ushiriki wa umma lililoanza leo Ijumaa Oktoba 4,2024, limeongezwa kwa siku moja zaidi. Zoezi hilo litaendelea hadi Jumamosi Oktoba 5,2024 saa kumi na moja jioni,” alisema Njoroge katika taarifa hiyo.

Njoroge aliwataka Wakenya kuhakikisha wanawasilisha maoni yao kuhusu suala hilo kufikia kesho Jumamosi.

Alisema afisi zote za maeneo bunge 290 zilizo chini ya tume ya utumishi wa huduma za bunge zitasalia wazi kesho ili kuwezesha shughuli hiyo kuendelea.

Haya yanajiri kufwatia agizo la mahakama kuu ya Kerugoya,kwa bunge la kitaifa kuandaa vikao vingine vya ushirikishwaji wa umma katika kila eneo bunge kuhusu hoja ya kung’atuliwa mamlakani kwa naibu rais Rigathi Gachagua.

Jaji Richard Mwongo alisema kikao cha ushirkishwaji umma kinachofanyika leo kinaweza kuendelea kama hatua ya kwanza, lakini akawataka washtakiwa kwenye kesi hiyo kuandaa vikao sawia vya ushirikishwaji umma kwa wananchi katika maeneo bunge.

Wakati alipokuwa akitoa kutoa agizo hilo jaji Mwongo alirejelea maamuzi ya mahakama ya upeo ambayo yamekuwa kanuni za mwongozo katika suala la ushirikishwaji umma.

Agizo hilo lilifuatia ombi lililowasilishwa na mwakilishi wa kike katika kaunti ya Kirinyaga Jane Njeri Maina.

Jaji alimwagiza Njeri kuwataarifu washtakiwa kabla ya kesi hiyo kutajwa siku ya Ijumaa juma lijalo atakapotoa maagizo zaidi kuhusu kesi hiyo.

Share This Article