Shule ya wavulana ya Highway kutoka Nairobi ndio mabingwa wa Kitaifa wa mashindano ya soka baina ya shule za upili kwa mara ya kwanza, baada ya kushinda mabingwa wa Magharibi, Musingu mabao matatu kwa mawili mjini Kisii leo Alhamisi.
Timu zote zilionyesha mchezo wa haiba kuu na kupata bao moja kila moja katika muda wa kawaida na ule wa ziada licha ya beki na nahodha wa Highway kulishwa kadi nyekudi kwenye kipindi cha pili cha muda wa kawaida.
Kupitia mikwaju ya penalti, Highway inayoongozwa na kocha wa timu ya soka ya taifa ya akina dada( Harambee starlets) Beldine Odemba, ilivuna ushindi wa mikwajo mitatu kwa miwili. St.Joseph ya Bonde la Ufa illibuka ya tatu nao Humphrey Aroko ( Highway) na Anorld Shivachi ( Musingu) wakaibuka mchezaji na mlinda lango bora mtawalia wa soka ya wavulana.
Katika soka ya wasichana, Mabingwa watetezi Butere kutoka eneo la Magharibi, wamehifadhi taji hilo kufuatia ushindi wa magoli mawili kwa nunge dhidi ya wenyeji Nyakach huku mshambulizi wa timu ya taifa ya soka ya wachezaji wa chini ya umri wa miaka 17 Lorna Faith akipachika la Kwanza.
Kipusa huyo pia alituzwa kama mchezaji bora naye Mercy Akoth ( Nyakach) akawa mlinda lango bora. Timu ya St.Joseph ilitosheka na namabari tatu.
Kwenye Voliboli ya wavulana, Cheptil walinyakua taji kwa kuwalemea Namwela kwa seti tatu kwa mbili nazo Nyabondo na Hospital Hill zikaridhika na nafasi ya tatu na nne mtawalia.
Kwa upande wa akina dada, Kwanzanze waliilaza Kesogon seti tatu kwa mbili. Soweto na Lugulu waliibuka namabari tatu na nne mtawalia.
Kwenye mchezo wa Pete, Oyugi Ogango walifadhi taji hilo nao Bumala Ac, Andersen na Kinale wakimaliza wa pili,tatu na nne mtawalia.
Timu hizi zitawakilisha taifa katika michezo ya Afrika Mashariki baina ya shule za upili (FEASSSA) mjini Mbale nchini Uganda kuanzia tarehe 16 hadi 28 mwezi huu.