Bodi ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu, HELB imetangaza kuanza kupokea maombi Juni 15 mwaka huu.
Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amefichua hayo akiongeza kuwa wale watakaofaulu kupewa mikopo hiyo watajuzwa ifikiapo tarehe 31 mwezi ujao.
Machogu pia amesema kuwa kati ya watahiniwa 201,146 wanaostahili kujiunga na vyuo vikuu, 153,274 wamewekwa na mamlaka ya kutoa nafasi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu, KUCCPS katika programu mbalimbali za shahada katika vyuo hivyo.
Ameongezea kuwa shahada za vyuo vikuu zitafadhiliwa kupitia vipengele vitatu ambavyo ni udhamini, mikopo na malipo ya wazazi.
Waziri huyo amefafanua kuwa ada ya kila mwanafunzi itajulikana baada ya matokeo ya maombi ya ufadhili kutolewa, akiongezea kuwa ufadhili utatolewa kulingana na kiwango cha uhitaji.
Zaidi ya hayo, Machogu ameagiza vyuo vikuu na mashirika ya ufadhili kuanza uhamasishaji wa wanafunzi, wazazi na wadau mbalimbali kuhusu jinsi ufadhili utatekelezwa.
Vyuo vikuu pia viliagizwa kuwaarifu wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza, kuhusu kiasi kitakacholipwa na wazazi wao, baada ya matokeo ya maombi ya ufadhili kutolewa.