Hatuna mamlaka ya kuchunguza wanajeshi wa Uingereza, yasema EACC

KBC Digital
2 Min Read

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC imethibitisha kuwa Kikosi cha Jeshi la Uingereza Kinactotoa Mafunzo nchini Kenya (BATUK) hakipo chini ya mamlaka yake. 

Hii ni licha ya tume hiyo kupokea malalamishi mengi yaliyowasilishwa dhidi ya kikosi hicho.

EACC imebaini hili wakati ambapo Kamati ya Bunge la Taifa ya Ulinzi, Ujasusi na Uhusiano wa Kigeni inafanya uchunguzi kuhusiana na madai ya mienendo mibaya na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya BATUK.

Wakati wa mkutano kati ya kamati na tume hiyo, EACC ilifichua kuwa awali ilipokea ripoti tatu zikidai kufanywa kwa makosa mbalimbali ukiwemo ukabila, ufisadi na mizozo ya kikazi yanayowahusisha maafisa wa BATUK. Hata hivyo, tume iliyachukulia masuala hayo kuwa yaliyo nje ya mamlaka yake.

Awali, kamati hiyo ikiongozwa na Naibu Mwenyekiti Bashir Abdullahi ambaye pia ni mbunge wa Mandera Kaskazini ilikutana na wawakilishi wa chama cha wakongwe wa Mau Mau na Tume ya Kutetea Haki za Binadamu, KHRC na pia wakazi wa kaunti za Laikipia, Isiolo na Samburu.

Wanachama wa kamati hiyo walipendekeza kuwa EACC inapaswa kupendekeza sheria kufanyiwa marekebisho yatakayoiruhusu kutekeleza wajibu wake katika utekelezaji wa makubaliano ya kibiashara, kiuchumi na mashirika.

Kamati ya Ulinzi imekuwa ikichunguza madai ya ukabila, ukiukaji wa haki za binadamu na mashaka ya usalama yanayohusiana na operesheni za BATUK.

Uchunguzi huo unafuatia mashaka yaliyoibuliwa na umma juu ya mienendo ya wanajeshi wa Uingereza humu nchini hasa katika kaunti za Laikipia na Samburu.

KBC Digital
+ posts
Share This Article