Rais William Ruto ametangaza hatua muhimu ambazo serikali yake inalenga kutekeleza, ili kutatua maswala yaliyoibuliwa yanayokumba taifa hili.
Akizungumza leo Ijumaa baada ya kutangaza nusu ya kwanza ya Baraza la Mawaziri, Rais alitangaza kuwa serikali itaanza kutekeleza mara moja mipango itakayoshughulikia changamoto za kiuchumi na kijamii zinazoathiri maisha ya wakenya.
Alikariri haja ya kuharakisha utekelezaji wa mipango ya kuimarisha uzalishaji wa chakula na hatua zingine za kupunguza gharama ya maisha.
Kiongozi huyo wa taifa aliangazia kuhusu upanuzi wa mipango ya kuongeza nafasi za ajira na kuchukua hatua zingine mpya za kukabiliana na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Vile vile alisisitiza haja ya mdahalo wa umma kuhusu usimamizi wa raslimali za umma.
“Ipo haja ya mazungumzo ya umma kuhusu uvumbuzi, uwazi na uwajibikaji katika utumizi wa rasilimali za umma na kupunguza matumizi ya serikali,” alisema Rais Ruto.
Ruto aliahidi kubuni serikali inayowajumuisha wote kutoka sekta mbali mbali katika kufanya marekebisho ya kitaifa.
“Ni muhimu kubuni serikali jumuishi itakayotoa fursa kwa wananchi kutoka sekta zote ili kupeleka mbele mageuzi ya kitaifa,” alidokeza Rais Ruto.